Monday, June 9, 2014

HABARI KUHUSU MAREHEMU MZEE SMALL.




Msiba tena! Ukweli ni kwamba gwiji wa maigizo na vichekesho Bongo, Said Ngamba ‘Mzee Small’ ameandamwa na roho wa kifo kwa siku 790 hadi alipokutwa na umauti usiku wa kuamkia jana, Ijumaa Wikienda lilikuwa naye bega kwa bega.



Mzee Small aliyekuwa na umri wa miaka 59, anakuwa mwigizaji wa nne kufariki dunia ndani ya siku 21 akitanguliwa na Adam Phillip Kuambiana, Sheila Leo Haule ‘Recho’ na George Otieno Okumu ‘Tyson’ ambaye bado hajazikwa huku kwenye michezo kukiwa na pigo la kuondokewa na Ally Hassan Mwanakatwe na Gebo Peter.




ALITESEKA SIKU 790
Kabla ya kukutwa na mauti kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar, Mzee Small aliteseka kwa miaka miwili na miezi miwili, jumla ya siku 790, ambapo alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi au kupooza (stroke).
Katika kipindi hicho chote Mzee Small alikuwa akiteswa na maumivu ya ugonjwa huo unaosumbua wengi kwa sasa ambapo alikuwa akilazwa mara kwa mara.

Kwa mujibu wa mwanaye aitwaye Mahamud Said, Alhamisi iliyopita Mzee Small alikuwa akitaniana naye lakini ilipofika usiku hali ilibadilika na akawa anakoroma kupita siku za kawaida.
Alisema kulipokucha siku ya Ijumaa hali ilizidi kuwa mbaya hivyo ndugu, jamaa na marafiki walimkimbiza Muhimbili alikokutwa na mauti.

TABATA-MAWENZI
Mahamud alisema mbali na kukoroma, Mzee Small, akiwa nyumbani kwake Tabata-Mawenzi, Dar alikuwa hazungumzi huku akitokwa na damu mdomoni hadi alipokutwa na mauti majira ya saa 4:00 usiku wa siku hiyo.

ALITENGWA NA BONGO MOVIES?
Enzi ya uhai wake wakati anaumwa, msanii huyo aliwahi kuandikwa na gazeti hili huku wasomaji wakiombwa kumchangia baada ya kudai kutengwa na wasanii wenzake wa filamu za Kibongo ‘Bongo Movies’.

Mwezi Machi, mwaka huu, mkongwe huyo aliliambia Ijumaa Wikienda kuwa ugonjwa wa kupooza ulimuanza tangu Mei, mwaka 2012 ambapo ulikuwa ukimsumbua kiasi cha  kushindwa kufanya shughuli zake za kawaida kwani alikuwa ni mtu wa kushinda ndani.
“Siwezi kutembea kwa zaidi ya miaka miwili, nimekuwa mtu wa kulala kitandani tu, nikitaka kuelekea chooni mke wangu ndiye ananisaidia,” alisema Mzee Small kwa uchungu.
ALIWASHUKURU WASANII
Mzee huyo aliyeonekana kuwa dhaifu, alisema anawashukuru baadhi ya wasanii ambao walikuwa pamoja kwa kumpa misaada mbalimbali lakini pia aliwazungumzia wale ambao walimtenga kipindi chote cha kuugua.
“Ninaposikia wasanii wanasema kwamba kuna umoja, napinga hilo. Kuna watu wengi nimefanya nao kazi na hata wengine kuwatoa mikoani na kuja Dar kwa ajili ya kufanya kazi, wakafanikiwa lakini siwaoni katika kipindi chote cha kuteseka kwangu kitandani,” alisema Mzee Small.
Endapo angepona, aliahidi kurudi tena katika uwanja wa maigizo kwa kutoa filamu kadhaa mwaka huu kwani alisema anajiona kuwa na nguvu za kufanya kazi tena.
Bila kujua mbeleni alisema: “Narudi. Wale walioanza kunisahau nawaambia kwamba nitarudi tena na kutoa kazi nyingi zenye mafundisho.”
MAZISHI
Habari zilizopatika wakati tunakwenda mitamboni jana zilieleza kuwa mazishi ya staa huyo wa komedi Bongo, yatafanyika leo kwenye Makaburi ya Segerea, Dar kama wosia wake ulivyoeleza na siyo kijijini kwake Kilwa, Pwani alikozaliwa akitokea  Kabila ya Wamatumbi.
Baadhi ya kazi za sanaa alizofanya ni pamoja na michezo ya runingani ya Hamsini Hamsini Mia, Nani Mwenye Haki, Mjini Shule na mingine kibao, baadhi ya michezo hiyo aliitolea filamu zilizopendwa na wengi.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.
Makala kamili funua ukurasa wa 7.





No comments: