MUIGIZAJI mwenye mvuto wa kipekee Bongo, Elizabeth Michael Kimemeta ‘Lulu’ juzikati alimsapraizi staa mwenzake wa sinema za Kibongo, Mahsein Awadh ‘Dk. Cheni’ pale alipomfuata mbele na kummwagia Dola za Marekani kiasi ambacho hakikujulikana mara moja
Lulu alifanya tukio hilo mbele ya watu kibao, katika sherehe ya maadhimisho ya siku ya kuzaliwa (birthday party) ya Dk. Cheni ikiwa ni pongezi zake kwa staa huyo kufikisha miaka kadhaa tangu alipoiona dunia.
Tukio hilo lililomshtusha Dk. Cheni lilitokea Julai 20, 2014 kwenye Ukumbi wa Ngorongoro uliopo ndani ya Hoteli ya Lamada, Ilala jijini Dar es Salaam.
Katika tukio hilo, Dk. Cheni aliambatanisha na shughuli ya kuwafuturisha mastaa wenzake na wadau mbalimbali wa sinema Bongo katika Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani
MWANZO WA TUKIO
Ilidaiwa kuwa, Dk. Cheni kwa kuwa aliamua kuitumia nafasi ya kufuturisha siku hiyo na kusherehekea bethidei yake, alijipanga vilivyo kuhakikisha kila mhudhuriaji anafurahia uwepo wake kwenye shughuli hiyo.
Miongoni mwa mastaa waliohudhuria mbali na Lulu ni pamoja na msanii wa nyimbo za kughani mashairi, Mrisho Mpoto, Vincent Kigosi ‘Ray’, Salum Mchoma ‘Chiki’, William Mtitu, Jacob Stephen ‘JB’ na Yobnesh Yusuph ‘Batuli’.
Wengine ni mkongwe kwenye Bongo Fleva, Joseph Haule ‘Profesa Jay’, Halima Yahya ‘Davina’, Wastara Juma, komediani Hemedi Maliyaga ‘Mkwere’, Kulwa Kikumba ‘Dude’, mwimbaji wa Injili, Emmanuel Mbasha (anayelishwa keki) na wengine wengi
ILIKUWAJE?
Ni baada ya futuru kumalizika ndipo wakati wa shamrashamra za bethidei zilipounga ambapo Chiki aliyebeba jukumu la u-MC aliwatangazia watu kwamba, miaka kadhaa nyuma, tarehe 20, Julai, Dk. Cheni alizaliwa jijini Dar es Salaam.
FURAHA, PONGEZI
Kuanzia hapo, furaha za kumbukumbu hiyo ziliibuka na kwa vile watu walikuwa wameshiba, waliweza kumpa pongezi Dk. Cheni kwa kumfuata mmojammoja alipokuwa amesimama na mke wake, Sabra wakitumia staili mbalimbali kwa kila mmoja alivyotaka lakini bila kuvunja maadili
Wengi walimpongeza kwa kumkumbatia au kumpa mkono wa heri ulioambatana na zawadi mbalimbali zikiwemo fedha.
LULU ASIMAMA, AENDA KWA DK. CHENI
Lulu ambaye amezoea kumwita Dk. Cheni baba, naye alisimama na kumfuata ‘mtoto’ Cheni ili kumtunza kwa alichonacho.
Macho ya wengi yalitarajia kumuona Lulu amebeba mzigo wa zawadi lakini walipogundua hana, waliamini angetuza kwa noti za ‘Msimbazi’ ambazo zinatumika Bongo, matokeo yake akaanza kuchomoa dola katika ‘waleti’ yake ya kike na kumtupia
DK. CHENI ATOA NENO
Baada ya kuona zawadi hiyo, Dk. Cheni ambaye alivaa kanzu yenye rangi ya maji ya maharage alijikuta akizidiwa na furaha kiasi cha kukaribia kumwaga machozi.
Katika kuonyesha furaha yake, Dk. Cheni alifunguka: “Jamani Lulu utaniua baba yako. Ni mambo gani hayo unanifanyia ya kushtukizana
LULU ASAKWA NA MAPAPARAZI
Baada ya shughuli hiyo kumalizika, mapaparazi wa Risasi Mchanganyiko walimfuata Lulu na kumuuliza dola alizompa Dk. Cheni zina thamani ya shilingi ngapi za Kitanzania.
Hata hivyo, nyota huyo alikataa kuweka wazi akisema ni siri ya aliyepewa.
“Hiyo ni siri ya Dk. Cheni mwenyewe, mimi nitasema nini sasa jamani?”
Mapaparazi walimfuata Dk. Cheni na kumuuliza ambapo aliminya idadi kamili ya fedha alizotoa Lulu na Mpoto akisema ni siri yake na mke wake